Wataalamu wa Afya Waonya Dhidi ya Matumizi ya Cetirizine kwa Lengo la Kubana Uke

 


Katika siku za hivi karibuni, mitandao ya kijamii imekumbwa na mwenendo wa kusambaa kwa madai kwamba vidonge vya Cetirizine, dawa inayotumika kutibu mzio (aleji), vinaweza kutumiwa kwa kuviingiza ukeni ili kufanya uke ukauke na hivyo kuleta hali ya kubana wakati wa tendo la ndoa.

Madai hayo yamesababisha tahadhari kutolewa nchini Kenya na Chama cha Wafamasia Kenya (Pharmaceutical Society of Kenya – PSK) pamoja na Mamlaka ya Dawa na Sumu (Pharmacy and Poisons Board – PPB), ambazo zimeonya dhidi ya matumizi hayo kutokana na kutokuwa na ushahidi wa kisayansi unaothibitisha usalama au ufanisi wake.

Kwa nini matumizi hayo ni hatari?

Cetirizine ni dawa ya kundi la antihistamine inayotumika kupunguza dalili za mzio kama kupiga chafya, mafua ya mzio (aleji), kuwashwa kwa macho na ngozi pamoja na vipele vya mzio (aleji). Dawa hii imetengenezwa kwa ajili ya kumezwa kupitia mdomoni, si kuingizwa ukeni.

Kwa nini matumizi hayo hayashauriwi?

Kwa mujibu wa mamlaka za afya nchini Kenya, Cetirizine haijaidhinishwa kwa matumizi ya ukeni wala kwa lengo la kubana uke. Hakuna ushahidi wa kisayansi unaothibitisha kuwa matumizi hayo yanaweza kufanikisha lengo hilo. Aidha, vidonge hivyo vimetengenezwa kwa ajili ya kumezwa, hivyo kuviingiza ukeni kunaweza kusababisha madhara kama muwasho, hali ya kuungua, maumivu na kuathiri mazingira ya kawaida ya uke.

Ushauri wa wataalamu

Wanawake wanashauriwa kutotumia Cetirizine au dawa nyingine za kumezwa kwa njia isiyokusudiwa na mtengenezaji au mtaalamu wa afya. Wenye changamoto za ukavu wa uke, maumivu wakati wa tendo la ndoa au masuala mengine ya afya ya uzazi wanapaswa kupata ushauri wa kitaalamu badala ya kufuata tiba zinazopendekezwa mitandaoni.

Kwa wale ambao tayari wamejaribu njia hiyo na kupata maumivu, kutokwa damu, kuwashwa, kuungua, uchafu usio wa kawaida ukeni au homa, wanashauriwa kutafuta huduma ya afya.

Kumbuka: Dawa kuwa inapatikana kwa urahisi kwenye maduka ya dawa haimaanishi kuwa ni salama kuitumia kwa matumizi tofauti na yale yaliyokusudiwa.