Kaswende ni ugonjwa wa maambukizi ya zinaa unaosababishwa na bakteria aitwaye Treponema pallidum. Mama mjamzito mwenye maambukizi haya anaweza kumwambukiza mtoto kupitia kondo la nyuma (placenta) wakati wa ujauzito. Hali hii hujulikana kitaalamu kama Congenital Syphilis (ikiwa na maana ugonjwa wa kaswende uliozaliwa nao).
Maambukizi haya yanaweza kusababisha madhara makubwa kwa mtoto, yakiwemo kuzaliwa kabla ya wakati, uzito mdogo, matatizo ya kiafya baada ya kuzaliwa au hata kifo cha mtoto kabla au muda mfupi baada ya kuzaliwa.
Jambo muhimu ni kwamba kaswende inaweza kutibika. Ndiyo maana wajawazito wanashauriwa kupima kaswende wanapohudhuria kliniki ya wajawazito na kupata matibabu mapema iwapo watagundulika kuwa na maambukizi. Matibabu sahihi kwa wakati yanaweza kuzuia maambukizi kwenda kwa mtoto na kupunguza madhara yake.
Kumbuka: Usisubiri dalili ndipo upime. Kupima kaswende wakati wa ujauzito ni sehemu muhimu ya kulinda afya ya mama na mtoto.
*Dokezo kuhusu picha: Picha iliyotumika ni ya kuwakilisha mada na haionyeshi dalili za kaswende
