Minyoo isipopatiwa dawa inaweza kuishi hadi miaka 50 ndani ya utumbo

Kuna aina ya minyoo inayoweza kuendelea kuishi ndani ya mwili wa binadamu kwa miongo kadhaa, hata zaidi ya miaka 50, bila kutibiwa.

Uwezo huu unatokana na mchakato wa kujizalisha upya ndani ya mwili unaojulikana kama autoinfection. Katika mchakato huu, mazalia ya minyoo hukomaa na kuingia tena kwenye ukuta wa utumbo, na hivyo kuendeleza maambukizi bila mtu kuhitaji kuambukizwa tena kutoka kwenye mazingira ya nje.

Maambukizi haya yanaweza kudumu kwa miaka mingi bila kuonyesha dalili. Hata hivyo, kwa watu wenye kinga dhaifu, yanaweza kusababisha ongezeko kubwa la minyoo mwilini na kusambaa kwenye viungo vingine, hali inayoweza kuhatarisha maisha.

Uwezo huu wa minyoo kuendeleza maambukizi kwa muda mrefu unaonyesha umuhimu wa kufanya vipimo mapema na kuzingatia matibabu sahihi ya minyoo.