Marekani kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani (FDA) imetoa ruhusa ya matumizi ya kipimo kipya kinachoweza kugundua Ebola, Marburg na virusi vingine vinavyosababisha homa kali za kuvuja damu, kwa kutumia sampuli moja ya mgonjwa.
Kipimo hicho kinachoitwa Xpert Hemorrhagic Fever Panel kina uwezo wa kugundua virusi vya Ebola, Marburg, Lassa na Crimean-Congo Hemorrhagic Fever (CCHF), huku kikitoa majibu ndani ya takribani dakika 61.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, kipimo hiki hutumia teknolojia ya PCR na kinaweza kugundua vinasaba vya virusi hivyo kupitia mfumo wa GeneXpert Dx.
Kwa upande wa Ebola, kipimo hiki kinaweza kugundua aina nne za virusi hivyo ambazo ni Zaire, Sudan, Taï Forest na Bundibugyo, lakini hakitofautishi aina hizo katika majibu yake.
Cepheid inaeleza kuwa kipimo hicho kinaweza kusaidia wahudumu wa afya kupata taarifa za haraka kuhusu uwepo wa virusi hivi, jambo linaloweza kusaidia kufanya maamuzi kuhusu kuwatenga wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na maambukizi, kuchukua hatua za kuzuia maambukizi na kutoa taarifa kwa mamlaka za afya ya umma.
Umuhimu wa kipimo hiki unatokana pia na ukweli kwamba dalili za awali za Ebola, Marburg, Lassa na Crimean-Congo Hemorrhagic Fever zinaweza kufanana na dalili za magonjwa mengine yanayosababisha homa, hivyo kufanya iwe vigumu kuyatofautisha kwa kutegemea dalili pekee.
Septemba 2026, kipimo hicho kilipata pia idhini ya matumizi ya dharura kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia utaratibu wa Emergency Use Listing (EUL).
Hata hivyo, kampuni imeeleza kuwa kipimo hicho hakipatikani katika kila nchi. Aidha, idhini ya FDA ni ya Marekani na haimaanishi moja kwa moja kuwa kipimo hicho kimesajiliwa au kinapatikana Tanzania.