Kenya imethibitisha kisa cha nane cha mgonjwa wa Ebola baada ya mwanaume mwenye umri wa miaka 49, aliyekuwa akifanya kazi za kusaidia wagonjwa katika Hospitali ya Nairobi (The Nairobi Hospital), kupatikana na maambukizi ya virusi hivyo.
Taarifa hiyo ilitolewa na Dkt. Patrick Amoth, Mkurugenzi
Mkuu wa Afya nchini Kenya, katika mahojiano na kituo cha televisheni cha
Citizen TV tarehe 18 Oktoba 2026. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwanaume huyo
hakuwa mhudumu wa afya anayetoa matibabu moja kwa moja, lakini kazi zake
zilihusisha kushughulikia vifaa vya wagonjwa, ikiwemo vyombo na mashuka.
Mgonjwa huyo alianza kuonyesha dalili zilizojumuisha homa,
maumivu ya kichwa na maumivu ya misuli. Vipimo vilivyofanyika vilithibitisha
kuwa alikuwa ameambukizwa virusi vya Ebola. Maelezo ya awali yanaashiria kuwa
huenda aliambukizwa kupitia mawasiliano yake na mgonjwa wa kwanza wa Ebola
aliyefariki katika hospitali hiyo tarehe 5 Oktoba 2026.
Kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa hadi wanane kunaibua swali
muhimu: Ebola inaweza kuenea vipi kupitia vifaa vya hospitali, na ni hatua gani
zinazoweza kuzuia maambukizi zaidi?
Ebola inaweza kuenea kupitia vifaa vya hospitali?
Ndiyo. Virusi vya Ebola vinaweza kuenea mtu anapogusana moja
kwa moja na damu au majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa. Maambukizi
yanaweza pia kutokea kwa kugusa vitu au sehemu zilizochafuliwa na majimaji
hayo, kisha virusi kuingia mwilini kupitia ngozi yenye jeraha au sehemu laini
za mwili kama macho, pua na mdomo.
Kwa mfano, mashuka, nguo, vifaa vya matibabu au vyombo
vinaweza kuwa chanzo cha hatari ikiwa vimechafuliwa na majimaji yenye virusi.
Hata hivyo, kugusa kitu ambacho kimehusishwa na mgonjwa
mwenye Ebola hakumaanishi moja kwa moja kwamba mtu ataambukizwa. Hatari
hutegemea kama kitu hicho kimechafuliwa na majimaji yenye virusi na kama virusi
vimepata njia ya kuingia mwilini kwa mtu aliyegusa.
Kufikia tarehe 18 Oktoba 2026, Kenya ilikuwa imethibitisha
wagonjwa wanane wa Ebola.
Mgonjwa wa kwanza alikuwa mwanaume aliyekuwa amesafiri
kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambako mlipuko mkubwa wa Ebola
unaendelea. Alifariki katika hospitali ya Nairobi tarehe 5 Oktoba. Baadaye,
watu wengine waliokuwa na uhusiano naye walipatikana na maambukizi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa, kati ya wagonjwa
walioambukizwa baada ya kisa cha kwanza, watatu walikuwa ndugu wa mgonjwa huyo
na wanne walikuwa wafanyakazi wa hospitali.
Mamlaka za afya zilikuwa zimeorodhesha watu 130 waliokua wamekutana
na wagonjwa walioambukizwa. Kati yao, watu 128 wamefikiwa na kufuatiliwa, huku
juhudi za kuwatafuta wengine wawili zikiendelea.
